Na VENANCE JOHN
Wagombea wenza katika kinyang’anyiro cha kuingia ikulu ya Marekani, Mdemokrat Tim Walz na JD Vance wa chama cha Republican wamepambana kwenye mdahalo wa makamu wa rais ambao ulikuwa wa kushangaza na wa kustaajabisha katika awamu ya mwisho ya kampeni ya uchaguzi iliyogubikwa na maneno ya uchochezi na majaribio mawili ya mauaji dhidi ya Donald Trump.

Wapinzani hao wawili, ambao wameshambuliana kwa nguvu kwenye kampeni, mara nyingi walipiga kelele, badala ya kuzungumzia sera za wagombea wao wakuu, Makamu wa Rais wa Demokrat Kamala Harris na Rais wa zamani wa Republican, Donald Trump.
Majibizano makali zaidi yalitokea karibu na mwisho wa mdahalo, wakati JD Vance, aliposema hangepiga kura kuthibitisha matokeo ya uchaguzi wa 2020, akijibu swali kuhusu kama angepinga kura ya mwaka huo ikiwa Trump atashindwa.
Walz alijibu kwa kulaumu madai ya uongo ya Trump ya ulaghai wa wapiga kura kwa kuanzisha umati wa watu Januari 6, 2021 ambao ulishambulia Bunge la Marekani katika juhudi ambazo hazikufua dafu kuzuia uidhinishaji wa ushindi wa Joe Biden wa 2020.
Walz, mweye mika 60, gavana wa kiliberali wa Minnesota na mwalimu wa zamani wa shule ya upili, na JD Vance, mwenye miaka 40, mwandishi na seneta wa kihafidhina kutoka Ohio, wameonesha namna maoni yao yanavyopingana sana juu ya masuala yanayosumbua nchi ya Marekani. Wapinzani hao walibishana kuhusu mgogoro wa Mashariki ya Kati, uhamiaji, kodi, uavyaji mimba, mabadiliko ya hali ya hewa na masuala ya uchumi.
Vance alihoji kwa nini Harris hakufanya zaidi kushughulikia mfumuko wa bei, uhamiaji na uchumi wakati akihudumu katika utawala wa Biden, akionesha kusisitiza kile ambacho Donald Trump mara nyingi alishindwa kukieleza kwa ufasaha wakati akikabiliana na Kamala Harris mwezi uliopita.
"Ikiwa Kamala Harris ana mipango mizuri kama hii ya jinsi ya kushughulikia shida za watu wa Marekani ya kati, basi anapaswa kuzifanya sasa, sio wakati wa kuomba kupandishwa cheo, lakini katika kazi ambayo watu wa Marekani walimpa miaka 3 na nusu iliyopita ameshindwa," Vance alisema.
Mjadala katika Kituo cha Matangazo cha CBS huko New York ulianza na mzozo unaoongezeka katika Mashariki ya Kati, baada ya Israeli kuendelea na mashambulio yake kusini mwa Lebanon siku ya Jumanne na Iran kufanya mashambulizi ya kulipiza kisasi dhidi ya Israel.
Trump, akitazama mdahalo huo kwenye runinga, alikuwa akichapisha kwa hasira, wakati mwingine mara mbili kwa dakika, kwenye mtandao wake wa Truth Social , akiwashambulia wasimamizi wa mdahalo huo uliorushwa na kituo cha CBS na kuwaita kuwa wenye huruma kwa Walz na wenye uelewa mdogo (IQ ya chini).
Comments