Na Ester Madeghe,
Maafisa wa Marekani na Urusi wanatazamiwa kukutana Jumanne mjini Riyadh kwaajili ya mazungumzo muhimu kati ya mahasimu wawili wa zamani wa vita baridi kuhusu kumaliza vita vya Moscow nchini Ukraine. Pande hizo mbili zinatarajiwa kujadili njia za kumaliza mzozo nchini Ukraine na kurejesha uhusiano kati ya Marekani na Urusi.

Mazungumzo hayo yanatarajiwa kufungua njia ya mkutano wa kilele kati ya Rais wa Marekani Donald Trump na mwenzake wa Urusi Vladimir Putin wakati pande hizo mbili zikijadili kurejesha uhusiano mzima wa Urusi na Marekani. Mkuu wa Hazina ya Utajiri wa Urusi siku ya Jumanne alimtaja Trump kama msuluhishi wa matatizo kabla ya mazungumzo ya Saudi Arabia.
"Kwa kweli tunaona kwamba Rais Trump na timu yake ni timu ya watatuzi wa matatizo, watu ambao tayari wameshughulikia changamoto kadhaa kubwa kwa haraka sana, kwa ufanisi mkubwa na kwa mafanikio makubwa," Kirill Dmitriev aliwaambia waandishi wa habari mjini Riyadh.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov atafanya mazungumzo na maafisa wakuu wa Marekani, akiwemo Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, ambayo yatalenga kumaliza vita vya Ukraine na kurejesha uhusiano chanya kati ya Urusi na Marekani .
Serikali ya Ukraine imesema hakuna makubaliano ya amani yanayoweza kufanywa kwa niaba yake katika mazungumzo hayo, ambayo Kyiv haikualikwa. Urusi inatumai kuwa Marekani itaiangalia nafasi ya Moscow katika mazungumzo kuhusu Ukraine, shirika la habari la Interfax lilimnukuu Dmitriev akisema.
"Biashara za Marekani zimepoteza karibu dola bilioni 300 kutokana na vita na uhasama wake na Urusi, hivyo kuna madhara makubwa ya kiuchumi kwa nchi nyingi, lakini tunaamini tutapata ufumbuzi",Dmitriev alisema.
Comments