Na VENANCE JOHN
Bunge la seneti nchini Ufaransa limeanza kujadili sheria ambayo itapiga marufuku uvaaji wa hijabu, kusujudu au kuwa na alama inayoashiria dini wakati wa mashidano ya michezo yote nchini humo.

Marufuku hiyo ambayo itahusu mashindano yanayoandaliwa na mashirikisho ya michezo, mashirika tanzu, ligi za kitaaluma na vyama tanzu pamoja na michezo ya kuogelea, ilianza kujadiliwa jana na mjadala huo utaendelea leo kabla ya kupigiwa kura na wabunge.
Wawakilishi waliopendekeza muswada wa marufuku hiyo wanataka kuwekwa marufuku ya alama za kidini katika sekta ya michezo, kwa madai ya kulinda uhuru wa serikali, katika hatua inayofanana na ile ya marufuku ya vazi la hijabu inayotumika katika shule za Ufaransa. Marufuku ya Seneti ya Ufaransa inakataza hata kusujudu kwa ajili ya kumshukuru Mungu baada ya kufunga goli
Marufuku hiyo ya Seneti ya Ufaransa ina maana kwamba wanamichezo Waislamu hawataruhusiwa kusujudu baada ya kufunga mabao, na wala hawataruhusiwa kufuturu uwanjani katika mwezi wa Ramadhani, kama ilivyokuwa ikifanyika awali. Mswada huo pia unapendekeza kupiga marufuku uwepo vituo vya ibada na maombi kwenye viwanja vya michezo au kuvaa mavazi ya kidini katika mabwawa ya kuogelea ya umma.
Shirika la kuteta haki za binadamu la Amnesty International limesema wabunge wa Ufaransa lazima wakatae muswada huo ambao wameuita wa kibaguzi ambao utapiga marufuku uvaaji wa nguo na alama zinazoonekana kuwa za kidini wakati wa mashindano ya michezo nchini Ufaransa.
コメント