Na Kulwa Mwaijulu
Watu zaidi ya 500 wanaweza kuwa waliteswa au kufa kwa njaa na kisha kuzikwa katika kaburi la siri la watu wengi kaskazini mwa mji wa Khartoum nchini Sudan.

Uchunguzi uliofanywa na gazeti la The Guardian la nchini Uingereza umeonyesha eneo kubwa la maziko lililopatikana katika kituo cha zamani cha Vikosi vya Msaada wa Haraka nchini Sudan (RSF), huku wafungwa waliookolewa wakizungumzia mateso, njaa na vifo vya wafungwa wenzao. Karibu na hapo palikuwa na eneo kubwa la kuzikia lenye takriban makaburi 550 ambayo hayajawekwa alama, mengi yakiwa mapya na inaonekana yalikuwa na miili mingi.
Awali katika eneo hilo palikua ni uwanja mkubwa zaidi wa kuzikia wakati wa vita vya wenyewe kwa wenyewe nchini Sudan. Ikiwa itathibitishwa, hiyo inaweza kuwa ni uhalifu mbaya zaidi wa kivita tangu kuanza kwa mzozo nchini humo.
Watu waliookolewa kutoka katika kituo cha kizuizini takriban kilomita 70 kaskazini mwa mji mkuu Khartoum wameeleza kwamba wengi walikuwa wamefia ndani na wanaaminika kuzikwa papo hapo. Uchunguzi wa miili mingi ya waliookolewa katika eneo hilo uliofanywa na madaktari ulionyesha dalili nyingi za kuteswa na kuhitimisha kuwa walikuwa wana njaa.
Comments