Watu watano wamepandishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni wakikabiliwa na mashtaka 23 likiwemo la kuongoza genge la uhalifu na wizi wa fedha kiasi cha Sh 3,600,000. Washtakiwa katika kesi hiyo ni Wangina Chacha (21), Erick Mushi (28), Shabani Msuya (36), Baraka Lunanja (32) na Kassim Dyamwale(34).

Wakili wa Serikali, Nitike Mwaisaka alidai hayo hapo jana tarehe 24 Septemba, 2024 alipokuwa akiwasomea washtakiwa hao mashtaka yao mbele ya Hakimu Mkazi Mfawidhi, Kemilembe Josiah washtakiwa hao walipofikishwa mahakamani hapo.
Mwaisaka alidai katika mashtaka ya kwanza ya kuongoza genge la uhalifu na kuingilia mfumo wa kompyuta kwa lengo la kufanya uhalifu linawakabili washtakiwa wote ikiwa walitenda kosa hilo Julai 28, 2024 wakiwa katika maeneo ya Mabibo Mwisho, Wilaya ya Ubungo Dar es salaam.
Aliendelea kudai kuwa Julai 28, 2024 katika eneo la Mabibo Mwisho Wilaya ya Ubungo mshtakiwa namba mbili na tatu walijiwasilisha kuwa ni wafanyakazi huru wa kampuni wa mtandao wa simu Airtel kwa Wilbard Simon wakijua kuwa sio kweli.
Pia Julai 28, 2024 washtakiwa wote wakiwa katika eneo la Mabibo Mwisho, waliingilia mfumo wa kompyuta kinyume cha sheria kwa kutumia namba ya simu ambayo mmiliki ni Pius Mpanduli.
Alidai kuwa kosa la kutumia kifaa haramu na kuingilia mfumo kinyume na sheria linawakabili mshtakiwa namba moja, mbili, nne na tano, kati ya Septemba 8 hadi 11, 2024 washtakiwa walikutwa wana kifaa kilichoitwa "Screen recorder Unlimited".
Comments