Kamanda wa Polisi Mkoa wa Rukwa, Kamishina Msaidizi Mwandamizi wa Polisi (SACP) Shadrack Masija, ametoa wito kwa wasafirishaji na wabebaji wa mizigo mkoani Rukwa kuhakikisha kuwa wanazingatia usalama wanaposafirisha mizigo yao kwa kutumia vyombo vya moto.

Ameyasema hayo Novemba 05, 2024, alipokuwa katika ziara ya kikazi Wilayani Nkasi, kwenye Kituo cha Polisi Namanyere. Akiwa hapo, alikagua hali ya kituo na kushuhudia tukio la mwananchi aliyekuwa anashikiliwa kwa kubeba mzigo kwa njia hatarishi, kinyume na sheria za usalama barabarani. Tukio hili limemchochea Kamanda Masija kuonya vikali dhidi ya tabia za uvunjifu wa sheria zinazohusiana na usafirishaji salama wa mizigo.
Kamanda Masija amesisitiza matumizi ya magari maalum yaliyoidhinishwa kwa kazi za kubeba mizigo, badala ya kutumia magari yasiyokidhi vigezo vya usalama. Ameeleza kuwa hii ni hatua muhimu ya kudhibiti ajali na kuimarisha nidhamu barabarani, akielekeza kuwa yeyote anayevunja sheria hizi hatasita kuchukuliwa hatua za kisheria.
Aidha, Kamanda Masija ametoa onyo kwa wavunjaji wa sheria za usalama barabarani na kuwataka kuhakikisha wanazingatia sheria kwa maslahi ya usalama wa wote. Amewakumbusha kuwa usafirishaji holela wa mizigo ni hatari kwa watumiaji wengine wa barabara na ni kosa la kisheria, hivyo ni muhimu kwa kila mmoja kufuata sheria ili kulinda maisha na mali.
Amewahimiza wananchi wa Mkoa wa Rukwa kushirikiana na Jeshi la Polisi katika juhudi za kudhibiti uhalifu kwa kutoa taarifa za kihalifu na wahalifu. Kamanda Masija amepongeza mchango wa wananchi katika kufanikisha jitihada hizi na amesisitiza kuwa ushirikiano huo ni muhimu katika kufanikisha malengo ya kuimarisha amani na usalama wa jamii nzima.
Commenti