top of page

NECTA YASEMA MWANAFUNZI ALIYENASA SAA 24 NDANI YA KIFUSI KARIAKOO ATAPATA USAIDIZI KUMALIZIA MITIHANI YAKE

NA VENANCE JOHN


Ombi la mwanafunziz wa kidato cha nne Jackson Clement, aliyenusurika kifo kwenye ajali ya ghorofa Kariakoo, limesikika baada ya Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) kumhakikishia hatapoteza haki yake ya kufanya mitihani aliyokuwa amebakiza.


Clement ni miongoni mwa manusura wa ajali ya kuporomoka kwa jengo la ghorofa nne, Kariakoo jijini Dar es Salaam, lililosababisha vifo vya watu 16 na majeruhi zaidi ya 86 na uharibifu wa mali zenye thamani ya mamilioni Novemba 16, 2024.


Clement ambaye ni mwanafunzi wa sekondari ya Charambe, alisimulia kisa chake kuwa huwa anakwenda kumsaidia shemeji yake siku za mwisho wa wiki, na kuwa siku anakutwa na mkasa huo alikuwa tayari ameshafanya mitihani saba ya kuhitimu kidato cha nne.


“Biology mmoja bado practical, nilikuwa na ombi kwa mwalimu wangu atafute namna yoyote ili nisaidiwe niweze kuufanya mtihani,” alisema Clement akiwa katika Taasisi ya Tiba ya Mifupa na Ubongo Muhimbili (MOl) anakoendelea na matibabu. Mitihani ya kidato cha nne, ilianza Novemba 11 na itamazika Novemba 29, 2024.


Leo Jumatano, Novemba 20, 2024, gazeti la Mwananchi limeripoti kuwa Katibu Mtendaji wa baraza la mtihani NECTA, Dk Said Ally Mohamed amesema mwanafunzi huyo hatapoteza haki yake ya kumaliza mtihani wake wa mwisho. “Ni mwanafunzi ambaye alikuwa na juhudi, ajali imetokea na yeye ikamkuta, lakini baraza litampa haki yake kadri inavyostahiki,” amesema.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page