Leo Jumatatu, mahakama ya Urusi imemhukumu raia wa Marekani Stephen Hubbard mwenye umri wa miaka 72, kifungo cha miaka sita hadi 10 jela, kwa kosa la kupigana kama mwanajeshi wa kigeni anayepigana katika taifa la Ukraine.

Hubbard, mwenye asili ya Michigan, alishtakiwa kwa kupigana dhidi ya Urusi kwa ajili ya fidia ya fedha na alikiri hatia mwezi uliopita kwa mashtaka ya kuwa raia wa Ukraine, hii ni kulingana na taarifa ziliyotolewa na vyombo vya serikali ya Urusi.
Waendesha mashtaka wa Urusi walidai kuwa Hubbard alipigana kama raia wa Ukraine katika mji wa Izyum, ikiwa ni sehemu ya kujipatia kipato, kwani alisaini mkataba wa takribani $1,000 kwa mwezi kwaajili ya kazi hiyo. “Ndiyo, nakubaliana na mashtaka,” Hubbard aliiambia Mahakama ya Jiji la Moscow mnamo Septemba 20, 2024 wakati kesi yake ilipokuwa ikisikilizwa.
Vivyo hivyo, leo Jumatatu, mahakama ya Urusi imemhukumu raia mwingine wa Marekani, aliyekuwa baharia Robert Gilman, kifungo cha miaka saba na mwezi mmoja jela kwa kuwashambulia maafisa wa kisheria.
Ikumbukwe kuwa, Gilman tayari anatumikia kifungo katika gereza la Urusi baada ya kuhukumiwa Oktoba 2022 zaidi ya miaka minne kwa kumshambulia afisa wa polisi, kulingana na Reuters. Adhabu yake baadaye ilipunguzwa hadi miaka 3.5. Hukumu ya Gilman iliyotolewa leo Jumatatu, katika jiji la Urusi la Voronezh, inahusiana na madai ya kumshambulia afisa wa gereza na mpelelezi wa serikali.
Comments