Na VENANCE JOHN
Maandamano yamezuka nchini Syria baada ya kuchomwa kwa mti wa Krismasi karibu na mji wa Hama. Video iliyosambazwa kwenye mitandao ya kijamii ilionesha watu waliojifunika nyuso zao wakichoma moto mti uliokuwa ukioneshwa kwenye uwanja mkuu wa Suqaylabiyah, mji wenye Wakristo wengi katikati mwa Syria.

Kundi kubwa la Kiislamu lililoongoza vuguvugu lililompindua Rais Bashar al-Assad limesema watu waliohusika na uchomaji huo walikuwa wapiganaji wa kigeni na wamekamatwa na kwamba mti huo utarekebishwa haraka. Maelfu ya waandamanaji wameingia barabarani kote nchini humo, wakitaka watawala hao wapya wa Kiislamu kulinda dini ndogo.
Katika kitongoji cha Bab Touma cha Damascus, waandamanaji walibeba msalaba na bendera za Syria, wakiimba "tutatoa dhabihu roho zetu kwa ajili ya msalaba wetu". "Ikiwa haturuhusiwi kuishi imani yetu ya Kikristo katika nchi yetu, kama tulivyokuwa zamani, basi hatuko hapa tena," mwandamanaji anayeitwa Georges ameliambia shirika la habari la AFP.
Syria ni nyumbani kwa makundi mengi ya kikabila na kidini, ikiwa ni pamoja na Wakurdi, Waarmenia, Waashuri, Wakristo, Druze, Alawite Shia na Sunni Waarabu, ambao wa mwisho wanaunda idadi kubwa ya Waislamu.
留言