Na VENANCE JOHN
Shughuli katika uwanja wa ndege wa Kenya wa Jomo Kenyatta zimetatizika baada ya wafanyakazi wa sekta ya usafiri wa anga kuanzisha mgomo hapo jana Jumanne usiku.

Wafanyakazi hao wanapinga mapendekezo ya kukodisha uwanja huo kwa miaka 30 kwa kampuni ya Adani kutoka nchini India. Shirika la ndege la Kenya, Kenya Airways limetoa taarifa kuelezea kutatizika kwa shughuli zake.
‘’Kwa sababu ya hatua zilizochukuliwa na wafanyakazi wa shirika la JKIA, hili limesababisha kuchelewa na hata kuahirishwa kwa baadhi ya safari za ndege zinazoingia na zinazotoka’’. Shirika hilo limesema katika taarifa yake.
Muungano wa wafanyakazi wa sekta hiyo awali ulikuwa umeonya kuhusu mgomo usio na ukomo baada ya serikali kushindwa kutoa maelezo ya mpango wa kukodisha uwanja huo. Foleni ndefu zilishuhudiwa huku mamia ya wasafiri waliokwama wakisubiri, na kuathiri shughuli za ndege katika uwanja huo wenye shughuli nyingi zaidi Afrika Mashariki.
Serikali ilisema kuwa mpango huo, unaojumuisha ujenzi wa njia ya pili ya ndege na kituo kipya, uko kwenye mkataba wa kampuni hiyo ya kibinafsi kujenga na kisha kuanza kuusimamia kwa kipindi cha miaka kadhaa. Pia ilifafanua kuwa bado hakuna uamuzi uliotolewa, lakini ukiidhinishwa, utatekelezwa ili kulinda maslahi ya taifa.
Hapo jana, mahakama kuu nchini humo ilizuia kwa muda mpango huo baada ya chama cha wanasheria nchini Kenya (LSK) na tume ya haki za binadamu kuwasilisha ombi, zikisema kuwa mpango huo haukuwa wa lazima, kwani Kenya inaweza kukusanya dola bilioni 1.8 zinazohitajika kuboresha uwanja huo wa ndege.
Comments