Na VENANCE JOHN
Serikali ya Kenya imekana kuhusika na madai ya kutekwa nyara kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Kizza Besigye. Siku ya jana Jumatano, mke wa Dr. Besigye, Winnie Byanyima, alidai mumewe alikuwa ametekwa nyara jijini Nairobi siku ya Jumamosi katika jumba moja katika eneo la Riverside Drive, na kusafirishwa mpaka Kampala nchini Uganda.

Katibu Mkuu wa Masuala ya Kigeni nchini Kenya, Sing’oei Korir, amesema, Kenya haina jukumu lolote katika madai ya kukamatwa au kufukuzwa kiongozi huyo mkongwe wa upinzani nchini Uganda. "Hakuna sababu yoyote kwa Kenya kuwa mshiriki katika kukamatwa kwake,’’ Korir alisema.
Besigye ameshindana na Rais wa Uganda Yoweri Museveni katika chaguzi nne na kushindwa mara zote, ingawa amekuwa akipinga matokeo ya chaguzi hizo. Kulingana na familia yake, Besigye alitekwa nyara jijini Nairobi na kupelekwa Uganda, ambako wanajeshi wanadaiwa kumshikilia.
Wakati huo huo leo, Dr. Kizza Besigye, amefikishwa katika Mahakama ya Kijeshi ya Makindye, nchini Uganda akiwa na mwenzake, Obedi Lutale, wamekanushwa mashtaka yanayowakabili ambapo amerejeshwa rumande hadi mpaka Desemba 2. Mahakama ya Kijeshi nchini Uganda inamshtaki Besigye kwa makosa manne ikiwemo kupatikana na silaha katika hoteli moja jijini Nairobi.
Comments