top of page

BILIONI 120 ZATUMIKA KUBORESHA HUDUMA ZA MAJI UBUNGO

Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) imetumia kiasi cha Bilioni 120 kuimarisha huduma za Majisafi na Usafi wa Mazingira katika Wilaya ya Ubungo kwa Wakazi takribani 345,164.


Hayo yamebainishwa na Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu DAWASA, Mhandisi Mkama Bwire katika kikao kazi kilichoandaliwa na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya ya Ubungo kilichozikutanisha Taasisi za Umma, Viongozi wa Serikali ,Wawakilishi wa Wananchi kwa lengo la kujadili mipango na mikakati katika kuimarisha huduma za kijamii na maendeleo.


Mhandisi Bwire amesema kuwa Mitaa yote 34 katika Wilaya ya Ubungo imefikiwa na Miundombinu ya Maji ya DAWASA ikiwa ni mpango wa Mamlaka wa utekelezaji wa Dira/Ilani ya Serikali ya kufikisha huduma kwa asilimia 95 Mijini 2025.


“Kwa kipindi cha Mwaka 2021 hadi 2025, DAWASA katika Wilaya ya Ubungo imewekeza kiasi cha Bilion 120 ambazo zimetumika katika shughuli mbalimbali za kuwapatia Wananchi huduma ya Maji ikiwemo ujenzi wa mtandao wa bomba kwa umbali wa Kilomita 400, kuongeza vyanzo vya kuhifadhi maji Lita Milioni 11 kupitia ujenzi wa Tanki la Maji Tegeta A na Tanki la Mshikamano alisisitiza Mhandisi Bwire


“Kwa upande wa huduma za Usafi wa Mazingira, DAWASA imekamilisha ujenzi wa vituo Sita vya huduma kwa Jamii katika maeneo ya Manzese, Shekilango, External, Makuburi, Mbezi na Mloganzila pamoja na ujenzi wa Mtambo wa kichakata Takatope unaoendelea katika eneo la Kisopwa” alisema


Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Ubungo ,Mhe Lazaro Twange amezipongeza Taasisi zinazohudumia Wilaya hiyo kwa kazi kubwa inayoendelea kutekelezwa na kusisitiza kuimarisha Mawasiliano baina ya Ofisi ya Mkuu waWilaya na Taasisi hizo za Umma.


"Nimeona tukutane kwa lengo la kufahamiana, kusikiliza mipango mikakati ya Taasisi zenu katika kuhudumia Wananchi ili tujenge uelewa wa pamoja katika kuiendeleza Ubungo yetu," alisema Mhe Twange.


DAWASA inahudumia Wilaya ya Ubungo kupitia Mikoa yake ya Kihuduma ambayo ni Ubungo, Kibamba, Magomeni, Kinyerezi, Makongo, Mabwepande na Tabata yenye Jumla ya Wateja 184,432.

Comments


Msasa Media
  • Instagram
  • Facebook
  • X
  • Youtube
  • TikTok

Follow, like, comment, and share

Tel. +255758379300
Mbezi Dar es saalam

bottom of page